8th November 2014
Email
Print
Athari za biashara hii ni nyingi lakini inasababisha usugu kwa maradhi na vifo na kuhujumu afya ya mtumiaji kwa kuwa anatumia fedha lakini haponi na matokeo yake ni kifo.
MADHARA
Matokeo mabaya katika eneo hili ni kutumia dawa lakini isiyokupa tiba hali inayojulikana kitaalamu kama Therapeutic failure.
Hali hii inatokea kwa sababu dawa zinashindwa kutimiza lengo la tiba kutokana na ama kuwa na kiasi kidogo cha dozi kilichomo ndani yake au hakuna dawa inayokusudiwa kuua vimelea vya maradhi yanayomsumbua mhusika licha ya kwamba anatumia dawa hizo.
Kwa ujumla dawa hizi bandia zikitumika zinashindwa kuleta tiba au kumponyesha mgonjwa kunasababisha pengine aache au kusimamisha matumizi ya dawa hiyo na kwenda kwenye dozi nyinginge na kwa ujumla kama mfuatano huo utakuwa ni wa kumeza dawa bandia ni wazi maisha ya mgonjwa yanatishiwa kwa vile hatapona.
Fikiria msomaji kuwa na taifa la watu wagonjwa wasiopona maradhi kila mmoja ana kifua kikuu (TB) isiyopona mwenye vichomi au nyumonia kadhalika haponi wakati homa ya tumbo, malaria na magonjwa ya njia ya mkojo (UTI) pamoja na maambukizi ya via vya uzazi (PID) nayo yanakuwa sugu na watu wanazidi kuumwa licha ya kutibiwa kwa gharama kubwa na wataalamu.
MADHARA KIKEMIKALI
Kuwapo kwa dawa bandia kunadhuru figo kwani inawezekana madawa hayo yanatengenezwa na kila kemikali bila kuzingatia viwango yanaishia kwenye figo za binadamu.
Sumu hizo zinasababisha madhara kwa watumiaji kwa mfano dawa za vikohozi zilidhuru watu wengi nchini Haiti, Bangladesh, Nigeria, India na Argentina .
Ni mifano kwa watu waliodhurika na kutumia dawa bandia ambazo licha ya kuwa feki zilikuwa na sumu na kuharibu figo zao. Lakini pia mwaka 2008 wagonjwa zaidi ya 62 walikufa nchini Marekani kutokana na kutumia dawa ya kusafisha figo iliyokuwa imetengenezwa China.
HUJUMA UCHUMI
Dawa feki au bandia ni hujuma kwa uchumi kwa vile idara za afya zinatumia fedha nyingi kuagiza dawa ambazo hazina tiba matokeo yake ni fedha kupotea , magonjwa kuchachamaa, nguvu kazi kudhoofika bila kusahau usugu wa vimelea.
KUSAMBAA DAWA BANDIA
Chanzo kikuu cha kusambaa dawa hizo ni rushwa. Kampuni za dawa na mamlaka za kiserikali zinazohusika na usimamizi wa uzalishaji, uuzaji na uagizaji wa dawa kuongozwa na watu wasio waadilifu ni chanzo cha tatizo hilo la kuenea rushwa kwenye sekta ya dawa. Ukosefu au kutegemea teknolojia duni kutambua maradhi vikiwamo vifaa vya maabara na wataalamu wanaojua kuchunguza na kutambua dawa feki ni eneo linakuza biashara haramu ya dawa feki.
Kukosekana utashi wa kisiasa kudhibiti biashara hiyo nako kunachangia. Hii ni dhahiri kwa sababu licha ya kuwa ni uhalifu wa kutisha na wenye madhara sawa na maangamizi haupigiwi kelele wala kuzungumziwa kama ulivyo uhalifu mwingine mfano matumizi ya dawa za kulevya na ugaidi.
Dawa bandia zinawekewa lebo feki kwa mfano unga wa mahindi unaweza kutengenezwa kama vidonge vya dawa inayotibu maradhi ya amiba na kwa makusudi ikabandikwa lebo na kuuzwa kama dawa wakati siyo,Dawa bandia ni biashara hatari ya sirini itafahamika na uchunguzi kuanzisha endapo vifo vitatokea kama hakuna janga inaendelea.
WAATHARIWA
Nchi changa ndizo zinazoumizwa zaidi kwa vile takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa karibu asilimia 50 ya dawa kwenye mataifa hayo ni bandia na katika nchi zilizoendelea ni kiwango kidogo cha asilimia moja,.
“Afrika na nchi za Asia zimeathirika zaidi na dawa hizo ripoti ya WHO mwaka 2005 ilikadiria kuwa kati ya asilimia 10 na 25 ya dawa zinazozunguka kwenye nchi hizo ni bandia”
Bara linaloumia zaidi ni Afrika likifuatiwa na Asia na Amerika ya Kusini
AINA ZA DAWA BANDIA
WHO inasema karibu kila dawa imetengenezewa dawa bandia kuanzia antibiotics (viuasumu), dawa za saratani, na zile za kutibu viungo vya ndani. Kwa nchi maskini athari ni mbaya zaidi kwa kuwa dawa bandia zinazosambazwa ni pamoja na antibiotics ambazo hutibu maradhi makubwa yanayoshambulia.
Kwa mataifa yaliyoendelea dawa feki zinazopatikana ni pamoja na za saratani, za kupunguza mafuta mwilini, dawa za mzio (aleji) za masuala yanayohusiana na vichochezi (homoni) pamoja na zile za kuongeza nguvu za kufanya ngono kwa upande wa wanaume.
Tiba feki za malaria zimesambaa mno eneo la Afrika na Asia zikiwamo hata zile za kufubaza makali ya Virusi Vya Ukimwi za VVU za ARVs.
Kwa hiyo wananchi wanapoona kuna kitu hawakielewi kuhusu au wanapozitumia dawa hawaponi, au zinanuka, pengine zinamomonyoka au zina kasoro kama kubadilika rangi, kutoa maji na kulowana waeleze taarifa kwenye mamlaka za kudhibiti ubora wa dawa.
Makala hii imetafsiriwa kutoka kwenye jarida la Research Journal of Medical Sciences.
SOURCE: NIPASHE
Comments
Post a Comment